Tarehe 31 Oktoba,2022, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo, alifanya mazungumzo na Bw. Simran Bindra, ambaye ni mmoja wa Wakurugenzi na Waanzilishi wa Kituo cha Kuchakata kokoa cha Kokoa Kamili kilichopo Kilombero, Morogoro, Tanzania. 

Katika mazungumzo yao, Bw. Bindra alieleza kuwa kokoa ya Tanzania inaendelea kunufaika na soko la hadhi ya juu Ulaya na Marekani na kwamba ni vema jitihada zaidi zikawekwa katika kuzalisha kokoa ya kiwango cha juu.

Mhe. Balozi Shelukindo alimpongeza Bw. Bindra kwa kazi nzuri ya kukuza uchumi wa Taifa kupitia zao la Kokoa. Aidha, amemshauri kuhakikisha kuwa anapiga hatua zaidi ili kuongeza thamani ya kokoa kwa kufikiria kuzalisha unga wa chokoleti nchini kwa matumizi ya ndani kama vile mahotelini na hata kwenye vyombo vya usafiri kama mashirika ya ndege. 

Bw. Bindra, yupo mjini Paris alipohudhuria maonyesho makubwa ya chokoleti yaitwayo "Salon du Chocolat" yaliyofanyika Paris tarehe 28 Oktoba hadi 1 Novemba 2022. 

Katika maonyesho hayo, watengenezaji na wauzaji mbalimbali wa chokoleti, wamesifu ubora wa kokoa ya Tanzania hususan kutokana na ladha yake ya kipekee.

Chokoleti hizo zinazotokana na kokoa ya Tanzania zinapatikana kwenye maduka mbalimbali nchini Ufaransa.