Mhe. Simai Mohammed Said, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali – Zanzibar, kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwasilisha hotuba kwenye Mkutano Mkuu wa 41 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), unaoendelea jijini Paris, Ufaransa. Mhe. Waziri alianza hotuba yake kwa kufahamisha msimamo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kuendelea kuunga mkono kazi za UNESCO kama njia ya kuimarisha diplomasia majumui (Multilateral Diplomacy).Mhe. Waziri alieleza kuhusu juhudi za nchi katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa misingi ya usawa baada ya kutokea Janga la UVIKO-19. Vilevile, Mhe. Waziri amepongeza jitihada za UNESCO katika kuwezesha Nchi Wanachama kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi na kueleza juhudi za nchi katika kuimarisha Sekta ya Ubunifu ambayo imeajiri Watanzania wengi, idadi kubwa ikiwa ni vijana. Mwisho, Mhe. Waziri alithibitisha nia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea na utekelezaji wa majukumu ya UNESCO sambamba na Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.