PARIS, UFARANSA – 23 Aprili 2026
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, amewasili salama jijini Paris tayari kuanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake ya kidiplomasia, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kimkakati kati ya Tanzania na Ufaransa pamoja na nchi anazowakilisha kwa makazi yake.
Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Charles de Gaulle Airport, Mheshimiwa Balozi Yakubu alipokelewa na Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa (Ministère de l’Europe et des Affaires étrangères), Bwana Florent Bourot, Afisa Mwandamizi wa Itifaki. Aidha, alipokelewa na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania wakiongozwa na Bwana Aggrey Meena pamoja na viongozi wa Umoja wa Watanzania wanaoishi nchini humo.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Mheshimiwa Balozi Yakubu alitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa imani kubwa aliyoonesha kwake kwa kumteua na kumpangia kituo hiki muhimu cha kidiplomasia nchini Ufaransa. Alieleza kuwa uteuzi huo ni heshima kubwa na dhamana nzito, na kuahidi kuifanya kazi hiyo kwa uadilifu, weledi na uzalendo wa hali ya juu ili kulinda na kuendeleza maslahi ya Taifa.
Aidha, alibainisha kuwa Ubalozi wa Tanzania jijini Paris utakuwa daraja muhimu la kuunganisha fursa zilizopo nchini na wadau wa Ufaransa na Ulaya kwa ujumla, huku akiahidi kushirikiana kwa karibu na diaspora ya Watanzania ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Ujio wa Mheshimiwa Balozi Yakubu nchini Ufaransa unatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda za kimkakati za Tanzania katika jukwaa la kimataifa, hususan kupitia ushiriki katika taasisi mbalimbali za kimataifa zenye makao yake Paris ikiwemo UNESCO.






